PENZI
Penzi njia ya adhabu, sina budi kuipita,
Tena ina nyingi tabu, ila siwezi iwata,
Leo naomba jawabu, ni lini nitakupata?
Tena ina nyingi tabu, ila siwezi iwata,
Leo naomba jawabu, ni lini nitakupata?
Penzi pia ni safari, ya hatari na salama,
Kuna wakati shuari, mara upepo wavuma,
Sote tuwe wasafiri, katu tusirudi nyuma.
Kuna wakati shuari, mara upepo wavuma,
Sote tuwe wasafiri, katu tusirudi nyuma.
Penzi ni kama misimu, iliyo ndani ya mwaka,
Kwa fuuza haidumu, kipupwe mara masika,
Kuna muda ufahamu, majani hupukutika.
Kwa fuuza haidumu, kipupwe mara masika,
Kuna muda ufahamu, majani hupukutika.
Penzi ni kama bahari, hutulia huchafuka,
Hupita mumo vihori, meli kubwa kadhalika,
Hivyo lataka hadhari, sivyo tupu kusumbuka.
Hupita mumo vihori, meli kubwa kadhalika,
Hivyo lataka hadhari, sivyo tupu kusumbuka.
Penzi mithili ya jua, huchomoza na kuzama,
Haya tusipoyajua, hakika twaenda kwama,
Hapa tamati natua, katika wako mtima.
Haya tusipoyajua, hakika twaenda kwama,
Hapa tamati natua, katika wako mtima.
Comments
Post a Comment