Skip to main content

Posts

NAKUPENDA EWE WANGU

 NAKUPENDA EWE WANGU 1. Wewe ndie nyota yangu,usiku wamulikia. Uniachi peke yangu,ukanacha ninalia.   Nikabaki peke yangu,mbali ukanikimbia.   Nakupenda ewe wangu,kwengine siwezi kwenda. 2. Wewe ndie mwezi wangu,usiku waangazia.   Ewe ndie taa yangu,mwanga wanimulikia.   Wewe ndie nuru yangu,wewe ndo langu pazia.   Nakupenda ewe wangu,kwengine siwezi kwenda.   3. Wewe ni asali wangu,nyuki sitowafukuza. Kuvunja mzinga wangu,ni jambo nisiloweza. Nikabaki peke yangu,ulimwengu kuniweza. Nakupenda ewe wangu,kwengine siwezi kwenda. 4. Ewe ndio shuka langu,lanilinda kwa baridi.   Wewe ndie koti langu,daima sitokaidi.   Takulinda vazi langu,ili nije kufaidi. Nakupenda ewe wangu,kwengine siwezi kwenda.
Recent posts

NIELEZE

NIELEZE nambie swahiba;nipate elewa kuchomwa na mwiba;si hadi kulewa kwa nini umevimba;mi sijaelewa..... nieleze!!! nambie habiba;nijue kwa nini kutwa umevimba;hatuelewani na hali mkosa;ni wewe si mimi nambie!!! kuwa na hiyana;si vema ujue alo muungwana;hafichi mwenziie alapo banana;humwita mwezie nambie!!

MIAKA ELFU

MIAKA ELFU Iwe miaka elfu, kipande cha kusubiri, Fahamu sinayo hofu, nakuacha ufikiri, Jibu lako kisharifu, nipa ukiwa tayari. Maili elfu moja, ni mbali nawe tuyuri, Nimo njiani nakuja, tena sinaye bairi, Hata yavimbe mapaja, siachi hii safari. Wawepo ndege alfu, nakupa moja nambari, Weye tuyuri furufu, kwako sinayo hiyari, Utaniingia ufu, jibu likiwa si zuri. Tamati kikwi si hoja, hili naomba kariri, Moyo wako naungoja, laili wa n'nahari, Uje ukae pamoja, na wangu kwenye suduri.

MPENZI RUDI NYUMBANI

MPENZI RUDI NYUMBANI 1. Mie nipo fikirani, mawazo yangu ya mbali, Sijui mkosi gani, nikaibinua stuli, Matone ya zafarani, katika kanzu na shali, Si urongo ni kweli, mwenzako sina amani. 2. Mekukumbuka fulani, usiku mie silali, Sijiwezi tabaani, siioni afadhali, Tonge halendi kinywani, zanipwaya suruali, Nimekonda kwelikweli, thama ni wewe jamani. 3. Siko vizuri kitwani, nenda rukwa na akili, Mwenzako kiza sioni, sipokuwa Ziraili, Roho yangu ishakani, kupona sina dalili, Sihitaji sipitali, namtaka wangu hani. 4. Mambo hayendi kazini, zimesimama shughuli, Hunitoki akilini, kutwa naona thakili, Naenda ovyo njiani, nikiwa na idhilali, Peke una ikibali, kupunga wangu shetani. 5. Nyonda hebu pulikani, sinitende ukatili, Hutotoka hatiani, roho ikiwacha mwili, Nakwambia si utani, hulikwepi zigo hili, Niikikata kauli, wapata faida gani? 6. Sita nafunga uneni, fahamu huna badili, Turudi kama zamani, makosa nayakubali, Nyongo mkalia ini, fahamu sinayo hali. Hebu fanya kulla hali, mpenzi rudi nyum...

PENZI

PENZI Penzi njia ya adhabu, sina budi kuipita, Tena ina nyingi tabu, ila siwezi iwata, Leo naomba jawabu, ni lini nitakupata? Penzi pia ni safari, ya hatari na salama, Kuna wakati shuari, mara upepo wavuma, Sote tuwe wasafiri, katu tusirudi nyuma. Penzi ni kama misimu, iliyo ndani ya mwaka, Kwa fuuza haidumu, kipupwe mara masika, Kuna muda ufahamu, majani hupukutika. Penzi ni kama bahari, hutulia huchafuka, Hupita mumo vihori, meli kubwa kadhalika, Hivyo lataka hadhari, sivyo tupu kusumbuka. Penzi mithili ya jua, huchomoza na kuzama, Haya tusipoyajua, hakika twaenda kwama, Hapa tamati natua, katika wako mtima.